Friday, March 11, 2011

Watendaji Moshi watiwa misukosuko

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali, jana iliendeleza makali yake kwa kuagiza watendaji wakuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, kukatwa asilimia 15 ya mishahara yao.Hatua hiyo ya kamati inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Agustine Mrema, inatokana na kile kichoelezwa kuwa ni kitendo cha watendaji hao, kuboronga katika kuandaa ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za miradi.

Juzi kamati hiyo, iliamuru watendaji 12 wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, wasimamishwe kazi na baadaye wakamatwe,kwa tuhuma za kuhusika na  upotevu wa mamilioni ya fedha.Watendaji walioamriwa kukatwa mishahara yao katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, ni pamoja na Mkurugenzi mtendaji, Annah Mwahalende.

Wengine ni Mtunza Hazina wa halmashauri, Evance Semdoe, wakuu wa idara na maofisa wanaosimamia miradi ya maendeleo.Adhabu kama hiyo ilitolewa Jumatatu wiki hii, kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, akiwamo mkurugenzi wake, Joseph Mkude.

Watendaji hao pia walituhumiwa kuboronga kazi ya kuandaa ripoti.Akitoa uamuzi huo,Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Idd Azzan, alielezea masikitiko ya kamati kuhusu ubovu uliojitokeza katika kuandaa na kuwasilisha ripoti ya halmashauri.

Kwa sasa halmashauri hiyo, imetakiwa kuandaa upya ripoti yae na kuiwasilisha ifikapo Aprili 11 mwaka huu.Imeamriwa kuwa vitabu vya ripoti hiyo, vikabidhiwe katika ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kamati hiyo pia imemwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kuwaonya watumishi wa chini yake kwa njia ya maandishi.Lakini wakati ikimtaka mkurugenzi afanye hiyo, nayo imeazimia  kuishauri mamlaka ya nidhamu ya mkurugenzi huyo, imuonye kwa njia kama hiyo.

Mkaguzi wa Kanda, Kihuti Asaria, alielezea kusikitishwa kwake juu ya taifa kutumia mabilioni ya fedha kuwalipa watumishi mishahara na kuwasomesha, lakini wanashindwa kuandika ripoti sahihi.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo,Joseph Selasini, alisema ni jambo la kusikitisha kuona halmashauri hiyo inaboronga katika kuandaa ripoti, wakati ikiwa na wasomi wenye shahada na shahada za juu.




No comments:

Post a Comment